2022 ulishamiri watu kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wenzao

3 miezi imepita 49

Hakuna wiki iliyoacha kusikika kuwapo kwa mauaji ya watu yakiwamo ya mume au mke kumuua mwezi wake sababu kubwa ikitajwa kuwa wivu wa mapenzi. Kila uchao makamanda wa polisi wa mikoa walikuwa wakipokezana kutoa taarifa za mauaji ya namna hiyo.

Mauaji ya kwanza yaliripotiwa kutokea mkoani Dar es Salaam baada ya Barke Rashid (30) kuawa Januari Mosi, huku tukio hilo likithibitishwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Tukio la pili lililothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, ni la kuuawa kwa mlinzi wa kiwanda kwa kupigwa shoka kichwani na mgongoni akiwa chumbani kwake, Januari 4.

Katika taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, ACP Marck Njera, ilielezea kutokea kwa mauaji ya mfanyabiashara Mussa Hamis, mkazi wa Kijiji cha Ruponda, Nachingwea Lindi, Januari 5.

Kama vile haitoshi, mwezi huo pia kuliripotiwa mauaji ya kikatili yaliyotokea Januari 10, 2022 eneo la Miches baada ya muuguzi wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Rufina Komba, kukutwa ameuawa nyumbani kwake.

Lakini pia Januari 17 kuliripotiwa  mauaji ya mwanamke anayetajwa kwa jina la Teresia Maliya mkazi wa Ilboru wilayani Arumeru mkoani Arusha aliyedaiwa kubakwa na kunyongwa hadi kufa.

Matukio hayo yalikuwa kama yamefungulia mengine, yakiwamo ya watu sita wa familia moja kuuawa kwa kukatwa na mapanga sehemu mbalimbali za miili yao Julai 3, katika Kijiji cha Kiganza mkoani Kigoma.

LHRC WATOA NENO

Kutokana na mauaji hayo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kiliweka wazi kuwa haki ya kuishi ndiyo iliyoongoza kukiukwa nchini katika mwaka huu wa 2022 ambao leo unafika mwisho.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, anasema katika maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu 2022, kwamba tathmini ya ufuatiliaji wa matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu inaonyesha kuwa matukio hayo yaliripotiwa na vyombo vya habari.

"Kwa mwaka huu tukitathmini kwa haraka haraka, haki za binadamu zilizovunjwa sana ni haki ya kuishi. Mauaji ya wenza yamekuwa mengi. Mauaji ya kujiua watu wenyewe yamekuwa mengi. Lakini pia, mauaji yanayotokana tu na imani za kishirikina yamekuwa mengi,” anasema Anna.

Anataja mauaji hayo kuwa ni ya watu watano wa familia moja Dodoma yaliyotokea Januari 23 katika kijiji cha Zanka, wilayani Bahi, ambao walikutwa wameuawa ndani ya nyumba yao, huku miili ikiwa tayari imeharibika.

Anasema Mei 28, mtu aliyetambulika kwa jina la Said Oswayo, alidaiwa kumuua mkewe Swalha Salum (28) kwa kumpiga risasi kadhaa, nyumbani kwao eneo la Mbogamboga, Buswelu wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.

Pia anasema Septemba 14, ziliibuka taarifa kutoka kitongoji cha Kibumbe, Kata ya Kiwira, Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya za mke, mume na watoto wawili kukutwa wamekufa ndani ya nyumba na miili yao ikiwa imeharibika.

"Novemba 23, 2022, Shani Yohana, mkazi wa Mbeya, alishikiliwa na polisi kwa madai ya kuwaua watoto wake wawili kwa kuwacharanga na mapanga hadi kufa, chanzo cha mauaji kikiwa hakijulikani," anasema.

MPANGO AKERWA

Kuendelea kwa mauaji hayo, kulimshutua Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango, na kuelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya mauaji vilivyokuwa vikitokea na kuagiza Jeshi la Polisi kuingilia kati.

Kutokana na hali hiyo, alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kuingilia kati haraka na kukomesha mauaji ambayo yalikuwa yakishuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akiwa katika kijiji ambacho mauji hayo yalitokea, Makamu wa Rais alitoa siku saba kwa IGP kuwakamata wote waliohusika na mauaji hayo. Alitaka mauaji hayo yafanyiwe kazi mara moja.

Makamu wa Rais alisema vyombo vya dola vifanye kazi, asibaki hata mtu mmoja, asakwe, wasakwe popote walipo, wachukuliwe hatua mara moja, huku akiitaka idara ya upelelezi ihakikishe wahusika wa mauaji wanabainika.

Waziri wa Mambo Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni naye aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari, akisema katika kipindi cha kuanzia Januari Mosi hadi 15,  matukio 22 ya mauaji yanayohusisha ndugu wa familia moja na wivu wa kimapenzi yameripotiwa, huku akiwataka viongozi wa dini kuisaidi serikali kuelimisha wananchi kuwa na hofu ya Mungu.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST