Azam yaanzisha msako pointi tisa Ligi Kuu Bara

2 miezi imepita 24

Mechi hizo haijalishi wanacheza nyumbani au ugenini, imeelezwa.

Matajiri hao wa Chamazi walipata ushindi katika mechi zake saba mfululizo kuanzia walipoifunga Simba bao 1-0, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Azam FC itashuka tena dimbani Desemba 5, mwaka huu kuvaana na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika ulioko Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Ofisa Habari wa Azam FC, Hashim Ibwe, alisema wachezaji wao walipewa mapumziko ya siku chache na sasa wamerejea kuendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi dhidi ya Maafande hao.

Ibwe alisema malengo yao ni kuvuna pointi tatu na kutimiza malengo na mipango ya kushinda mechi 10 mfululizo.

“Tayari tumefanikiwa kushinda michezo saba, sasa malengo yetu na nguvu ni kutafuta pointi tisa katika michezo mitatu iliyosalia kati ya saba ambayo tayari tumekusanya pointi 21, mechi tatu zilizosalia ni kumfunga Polisi Tanzania siku ya Jumatatu na kurejea nyumbani na alama tatu.

Baada ya mechi yetu na Polisi Tanzania tutarejea nyumbani kwa ajili ya mchezo wetu wa hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Maliamo FC, katika mchezo huo pia tunahitaji ushindi ili kufikia yale malengo yetu ya kutwaa kombe hilo,” alisema Ibwe.

Aliongeza baada ya hapo wataendelea kujipanga kwa ajili ya michezo miwili ya ugenini kwa kuwakabili Kagera Sugar ifikapo Desemba 16, mwaka huu na siku tano baadaye itawavaa Geita Gold FC.

Aliongeza wamejipanga kukutana na ushindani hasa katika mechi za ugenini  ambapo kila timu wanayokutana nayo inahitaji kubakisha pointi zake nyumbani.

Azam FC yenye pointi 32 iko katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo nyuma ya vinara Yanga yenye kiporo cha mechi moja wakati Simba yenye pointi 31 iko katika nafasi ya tatu.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST