Turay

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mohamed Buya Turay akiwa katika picha na mkewe (kushoto) kabla ya siku ya harusi, ambapo kaka yake (kulia), alisimama kama mume kwa niaba yake

Saa 2 zilizopita

Mchezaji wa kimataifa wa Sierra Leone, Mohamed Buya Turay, alikuwa amedhamiria sana kuonyesha jambo na kuleta mabadiliko katika klabu yake mpya ya Sweden kiasi cha hata kuikacha mwezi harusi yake Julai ili kujiunga na mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya na klabu hiyo ya Malmo.

Siku chache baada ya kupiga picha za kuelekea kwenye harusi yake, akiwa amevalia nguo za harusi mjini Freetown, Turay ilibidi awakilishwe kwenye sherehe ya harusi yake katika mji mkuu na kaka yake, kitu ambacho ni cha kawaida katika ndoa za Kiislamu.

Hii ni kwa sababu Malmo alitangaza usajili wake mnamo 22 Julai, siku moja kabla ya ndoa yake.

"Sikuwepo kwenye siku ya ndoa na sherehe kwa sababu Malmo waliniomba nije hapa mapema," aliambia gazeti la Sweden la Afton Bladet.

"Tulipiga picha mapema. Kwa hiyo inaonekana kama nilikuwepo lakini sikuwepo. Kaka yangu alibidi aniwakilisha kwenye harusi yenyewe."

Ingawa kaka yake Turay angeweza kumsitiri siku ya harusi yake, lakini asingeweza kumtetea mshambuliaji huyo katika ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa na la kiwango cha juu Ulaya.

Kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 "anafuraha" kwenda Sweden kujiunga na timu hiyo yenye mafanikio zaidi, hivyo kumruhusu kuwania ubingwa wa Ligi ya Europa.

Chanzo cha picha, Getty Images

"Ni ndoto kwangu kucheza Ligi ya Ulaya na Malmo," aliiambia BBC Sport Africa. Baada ya kuondolewa katika mechi ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa, Turay aliisaidia Malmo kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Europa ambapo wako Kundi D pamoja na Sporting Braga ya Ureno, Union Berlin ya Ujerumani na Union Saint Gilloise ya Ubelgiji.

Alicheza kwa zaidi ya saa moja katika mechi ya kwanza ya kichapo cha 2-0 dhidi ya Braga lakini hakuwepo katika mechi ya kichapo cha 3-2 huko Ubelgiji, na - baada ya kufunga mara mbili katika raundi ya tatu ya kufuzu dhidi ya F91 Dudelange ya Luxembourg - bado anatafuta bao lake la kwanza katika hatua ya makundi.

Bado hiyo linaweza kutokea leo Alhamisi jioni, wakati Malmo watakapowakaribisha Union Berlin.

Wanasema ligi ya Sweden ni nyepesi

Turay analijua vyema soka la Sweden, baada ya kutumia muda mwingi wa maisha yake bora ya soka katika nchi ya Scandinavia.

Mnamo 2019, akiwa kwa mkopo Djurgardens IF, alishinda taji la Allsvenskan na tuzo ya kiatu cha dhahabu cha ligi akiwa na mabao 15. "Ligi ya Sweden imenitambulisha," Turay alisema.

Ingawa nchi hiyo haiwezi kuorodheshwa miongoni mwa ligi bora zaidi barani Ulaya, iliyoorodheshwa ya 23 kati ya ligi 55 katika viwango vya shirikisho la soka la Ulaya, UEFA. Turay mwenye umri wa miaka 27 ana mtazamo tofauti sana. Maoni yake yamekuja baada ya kurejea Sweden mwezi Julai kujiunga na mabingwa Malmo kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu, baada ya hapo awali kuachana na Henan Songshan Longmen ya Ligi Kuu ya China kwa makubaliano.

Ushauri kwa Kallon nchini China

Chanzo cha picha, Getty Images

Turay alikuwa sehemu ya kikosi cha Sierra Leone kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Cameroon mapema mwaka huu, akicheza mechi zote tatu za timu yake dhidi ya Algeria, Ivory Coast na Equatorial Guinea.

Mchezaji mwenzake katika timu ya taifa, Issa Kallon, ambaye pia alicheza Kombe la Mataifa, alijiunga na klabu ya Ligi ya China ya Shanghai Port akitokea Cambuur ya Uholanzi baada ya Turay kuondoka China na kuelekea Malmo.

Mshambuliaji huyo, anasema Kallon lazima ajitume kikamilifu ndani na nje ya uwanja ili kuzoea maisha yake mapya katika taifa hilo la Asia.

“Ushauri wangu kwake ni kwamba anatakiwa kufanya kazi kwa bidii kuliko mtu yeyote katika timu yao ili kufanikiwa,” alisema. “Ninajivunia kwa hatua aliyofikia kwenda huko, amefanya jambo la busara kwa kuchukua familia yake na hiyo itamfanya aendelee kufanya vyema katika timu.

"Najua ni vigumu kuwa huko bila familia yako. Nilipitia mengi bila familia yangu kwa miaka minne iliyopita, lakini nashukuru Mungu nimeoa sasa."