Chadema yawekwa njiapanda

2 miezi imepita 61

By Waandishi Wetu

Dar es Salaam. Hatima ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa imekiweka njiapanda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

Hali hiyo inatokana na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan wa kutakiwa kusubiri ripoti ya kikosi kazi kujua hatima hiyo, wakati chama hicho kikisubiri matokeo ya mazungumzo ya maridhiano baina yake na chama tawala, CCM.

Wasiwasi wa viongozi na makada unajitokeza wakati chama hicho hakikujihusisha na masuala ya Kikosi Kazi wala kujitokeza mbele yake kutoa maoni.

Katika ujumbe wake alioutoa Alhamisi iliyopita, Rais Samia alisema “tupo katika hatua mbalimbali za kutanua wigo wa ushirikishwaji wananchi kwa kuzingatia mazingira yetu huku tukiongozwa na moyo wa maridhiano yanayotujengea usawa, mshikamano na umoja.

Aliongeza, “tusubiri maoni na mapendekezo ya Kikosi Kazi juu ya marekebisho ya sheria na kanuni hizo na kwamba suala hili litatolewa tamko siku chache zijazo.”

Siku mbili baada ya kauli hiyo, Kamati Kuu ya Chadema ilikutana jijini hapa ikiongozwa na mwenyekiti wake Freeman Mbowe, pamoja na mambo mengine kuzungumzia hali ya kisiasa.

Advertisement

Licha ya ajenda za kikao cha cha kikatiba kutowekwa wazi, chama hicho kiko katikati ya shinikizo la baadhi ya wananchama, viongozi na wadau wa siasa kuhusu hatima ya mazungumzo ya maridhiano kiliyoanza CCM.

Wakati upande mmoja ukisubiria kikosi kazi, wengine wanasubiri matokeo ya mazungumzo ya maridhiano.

Mmoja wa vigogo wa Chadema alilidokeza gazeti hili pamoja na mambo mengine, kuwa majadiliano baina yao na Serikali na makala ya Rais Samia kuhusu demokrasia lilikuwa suala la lazima kuzungumziwa katika kipindi hiki.

“Tumekuwa katika majadiliano na Serikali, ni wakati wa kufanya tathimini kidogo ya nini kinaendelea, kwani baadhi wanasema tujitoe kwani CCM inatuhadaa na haina dhamira njema,” alidokeza kigogo huyo bila kutaka jina lake litajwe.

Hata hivyo, kigogo huyo alisema “chama ni vikao. Sasa kupitia vikao tunajadilia masuala mbalimbali yenye manufaa kwa Taifa na chama chetu. Baadaye tutaujuza umma kuwa nini tumekubaliana.”

Katika makala aliyoitoa kwa vyombo vya habari Septemba 15, 2022, pamoja na mambo mengine, Rais Samia aliweka bayana kuwa “vyama vya Siasa vimekuwa vikidai kuruhusiwa kuendelea kufanya kazi za kisiasa, hususan, kufanya mikutano ya hadhara na wanachama wao.

“Serikali itumie fursa hii kueleza kwamba, Kikosi Kazi kinachoratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kimeendelea kusisitiza kutolewa kwa ruhusa ya kuendesha mikutano ya vyama vya siasa, ila wameonyesha wasiwasi kwenye sheria na kanuni zinazosimamia suala hilo,” alisema.

Kauli hiyo haikupokelewa vizuri na baadhi ya wafuasi wa Chadema, wakiwemo viongozi katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliweka makala hiyo ya Rais Samia kisha akaandika, “Mh. Rais @SuluhuSamia uliapa kulinda Katiba ya nchi na uliahidi kuheshimu utawala wa sheria. Kuondoa zuio haramu la #Mikutanoyahadhara hakuhitaji kusubiri kikosi kazi wala marekebisho ya sheria...

Mei 20, mwaka huu, Mbowe akiambatana na baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwemo Mnyika na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Saidi Issa walikutana na Rais Samia Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Viongozi wengine walioambatana na Rais Samia walikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eliezer Feleshi na maofisa wengine wa chama na Serikali.

Hata hivyo, mazungumzo ya kikao hicho hayakuwekwa wazi na haijaeleweka lini wangekutana tena, licha ya kuelezwa vingekuwepo vikao vingine vya maridhiano, vikiwemo vinavyoshirikisha vyama vingine.

Alipoulizwa Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka kuhusu madai hayo, alisema hata kama kikosi kazi sio cha kisheria, lakini kimekuwa ni njia ya majadiliano ya namna ya kufanya siasa.

“Siasa ni suala la kukubaliana. Tumshukuru mheshimiwa Rais kwa juhudi alizofanya, kwani miaka mitano iliyopita kulikuwa na Katiba na sheria, lakini hali haikuwa hivi. Tunachotaka ni kufanya siasa zenye tija,” alisema Shaka.

Wakati hayo yakiendelea, Chadema pia ikipata msukumo wa makada na wanachama ju ya operesheni zake katika maeneo mbalimbali nchini, huku baadhi ya makada wake wakikamatwa.

Wiki moja tu baada ya mkutano wa Rais na viongozi wa Chadema, viongozi wa Baraza la vijana wa chama hicho (Bavicha) akiwemo mwenyekiti wake John Pambalu walikamatwa na polisi wilayani Babati Mkoa wa Manyara wakiwa kijiweni wakijadili na vijana wenzao. Hata hivyo, baadaye waliachiwa.

Mapema mwezi huu makada wawili wa Chadema akiwamo Katibu wa chama hicho Wilaya ya Nyamagana, David Nyakimwe na mwanachama wa chama hicho, Oswald Mang’ombe walikamatwa na polisi wakiwa kwenye maandalizi ya mkutano.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya viongozi na makada wa Chadema wamekuwa wakieleza wasiwasi juu ya mazungumzo hayo.

Miongoni mwa viongozi wanaohoji ni mjumbe wa kamati kuu na mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema anayeishi uhamishoni Canada, aliyemwandikia mwenyekiti wa chama hicho katika ukurasa wake wa Twitter.

“Mwenyekiti nimefanya kazi na wewe kwa muda mrefu. Naujua moyo wako juu ya nchi, najua nia yako. Ninakiri kuwa umejitoa kwa ajili ya Tanzania. Tunapokuwa kwenye mazungumzo ya Tanzania bora muombe Mungu akuonyeshe hila.” aliandika Lema bila kufafanua.

Wawe makini

Akijadili suala hilo, Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mohamed Bakari amekitahadharisha chama hicho kuwa makini na kikosi kazi, kwani kinaweza kuwa njia ya kuchelewesha maridhiano.

“Chadema wako sahihi kususia kikosi kazi kwa sababu hakina uhalali wa kisheria na kikatiba kama vyombo vingine, lakini kama tunataka tu kufanya mazungumzo basi ni jambo la heri.

“Ni njia fulani ya kufikia maridhiano, kwa hiyo kama kuna jambo zuri tutaliona. Lakini kikosi kazi kisije kikawa ni mkakati wa kuchelewesha hayo maridhiano yenyewe,” alisema.

Kauli ya Profesa Bakari imeungwa mkono na mchambuzi wa siasa, Bubelwa Kaiza aliyesema, “kikosi ni jitihada binafsi ya Rais Samia, kukisubiri kikosi kazi ni sawa na kukubaliana na Rais kuongoza nchi kwa maoni yake binafsi.

“Kwa kuwa Chadema hawako kwenye kikosi kazi, waendelee na kazi zao kwa kuwa zinatambuliwa na sheria na Katiba,” alisema.

Source : Mwananchi

SHARE THIS POST