COVID-19 imekuwa na fundisho kubwa kwa nchi yetu na Afrika kwa ujumla- Tanzania

2 wiki zimepita 49

Tanzania imesema janga la ugonjwa wa COVID-19 limetoa mafundisho lukuki ikiwemo jinsi gani ya kushughulikia majanga yajayo ya kiafya sambamba na kujenga uwezo wa kitaifa na kikanda wa kuzalisha dawa, vifaa vya matibabu na chanjo dhidi ya magonjwa.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Phillip Mpango amesema hayo Alhamisi jioni wakati akihutubia Mjadala Mkuu wa mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA77 jijini New York, Marekani.

Amesema sambamba na hilo, “suala la Afrika kuwa limeenguliwa kwenye upataji wa chanjo, lilipatia msisitizo umuhimu nchi za Afrika kushirikiana kuzalisha na kukuza majawabu ya kiasili kupitia tafiti za pamoja na kisayansi na kitabibu.”

Makamu huyo wa Rais wa Tanzania amesema janga pia la COVID-19 limeibua umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye elimu ya afya ya umma, hususan elimu yak inga kwa kujenga uwezo wa mwili wa mtu kujikinga kwa kufanya mazoezi ya mwili, lishe bora na  mifumo ya maisha.

Amekiri kuwa ingawa usaidizi wa kimataifa kwa Afrika katika kukabili kusambaa kwa COVID-19 kwa kupatia vifaa vya uchunguzi, dawa, fedha na chanjo ulichelewa, ulikuwa muhimu katika kushinda vita dhidi ya janga hilo.

Kwa mantiki hiyo, “Tanzania inapenda kushukuru wadau wote wa maendeleo ambao wamekuwa wanashirikiana nasi katika kukabili janga na kuweka nchi katika njia chanya ya kujikwamua kutoka janga la COVID-19.”

Amesema kwa sasa Tanzania inaendelea na kampeni  ya chanjo na hadi tarehe 11 mwezi huu wa Septemba asilimia 60.56 ya watu wanaopaswa kupatiwa chanjo dhidi ya COVID-19 walishachanjwa.

Tabianchi na mazingira- Mpito kuelekea nishati salama

Makamu wa Rais wa Tanzania amegusia suala linalotakiwa hivi sasa la nchi kuhama kutoka nishati kisukuku na kuelekea katika nishati salama akisema serikali yake inapongeza hatua zote zinazochukuliwa kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Hata hivyo Dkt. Mpango amesema Afrika lazima ipatiwe muda wa kuelekea kwenye mpito huo kwa sababu idadi kubwa ya waafrika hawana nishati.

Kanuni iliyoanzishwa ya wajibu wa pamoja lakini kwa utofauti kwa kuzingatia uwezo lazima inapaswa kuzingatiwa.

Kwa mantiki hiyo « tunatoa wito wa kuondoa upinzani kwa utoaji wa fedha na utekelezaji wa miradi ya kuleta mabadiliko kwenye nchi zetu ambazo zinalenga kuvuna hifadhi yetu ya maji na nishati za ukaa kwa ajili ya nishati na matumizi mengine muhimu ili kushughulikia mahitaji yetu muhimu ya maendeleo.”

Source : UN Habari

SHARE THIS POST