Tangu kupata Uhuru kilimo kimekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, hii imesababisha kuikata minyororo ya wakoloni kwa haraka na kutoa fursa kwa watu kujiajiri na kuajiriwa.
Kilimo pia kimetoa fursa za ajira ya moja kwa moja kwa wataalam wenye ujuzi kama vile washauri, walimu au watafiti katika nyanja zao.
Pia kuna ajira za muda kama vibarua katika mashamba, usindikaji, uzalishaji, ufungashaji na idara za usafirishaji.
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya watu wanapata ajira katika sekta ya kilimo, iwe moja kwa moja au kwa njia nyingine, na uimara wa sekta ya kilimo unategemea uzalishaji wa mazao na upatikanaji wake.
Kilimo cha biashara, huchangia kuongezeka kwa mapato ya ndani kupitia michango ya kodi kwa serikali na kuwanufaisha wakulima kwa kutoa fursa za kuzalisha mapato.
Takwimu zinaonesha kuwa Sekta ya kilimo Tanzania inaingiza asilimia 30 ya mapato ya ndani, na kilimo cha biashara kupitia sekta ya usindikaji wa mazao ya kilimo kinakuza biashara kwa ujumla na kuwapatia wakulima soko mbadala la kuuza mazao yao moja kwa moja kwa wingi kwa viwanda vya ndani.
Zao la pilipili hoho limezidi kupata umaarufu kutokana na soko lake kuwa wazi na thabiti huku pilipili aina ya Mwendokasi zikifahamika zaidi.
Wakulima wanaolima zao hili la pilipili wameanza kuona mafanikio kutokana na kuongezeka kwa uhakika wa soko, ari ya ununuzi na usimamizi mzuri.
Wakulima waliohojiwa na timu ya waandishi wa habari kutoka Kituo cha Vyombo vya Habari dhidi ya Umaskini (Me-CAP) wanasema zao la pilipili linakuwa kwa kasi na kuwa fursa kwao na limeondoa makali katika maisha yao.
MeCAP katika ziara yao walitaka kuchunguza jinsi wananchi wanavyonufaika na mazao ya biashara ili kupunguza umaskini, na jinsi kilimo cha pilipili Mwendokasi kinavyowasaidia wakulima.
Mikoa ya Arusha, Dodoma, Morogoro, na Iringa ilihusishwa na kote kulionekana pilipili Mwendokasi imeleta mageuzi katika biashara na kuwa chanzo kizuri cha kuwainua wakulima kiuchumi.
Baadhi ya wakulima wanasema kuna faida kubwa kutoka katika kilimo cha pilipili mwendokasi na kuchochea uchumi wao wa kila siku.
Uwepo wa kiwanda cha Darsh Industries Limited kama soko la kutegemewa umeibua shauku ya wakulima katika aina mpya ya zao la pilipili.
Darsh Industries Limited hununua na kusindika pilipili hizo kwa njia ya kisasa kupitia vifaa vyao vya hali ya juu vilivyoidhinishwa na taasisi ya kudhibiti ubora ya ISO.
Salum Mashaka mkazi wa Morogoro anayelima pilipili anaeleza kuwa imekuwa ni baraka kwake kuwa mmoja wa wakulima kwanza wanaonufaika na zao la pilipili mwendokasi tangu alipoanza kulima zao hilo kibiashara.
“Kwanza nitapata mbegu zenye ubora wa hali ya juu na kupata soko la uhakika kwa sababu kampuni ya Darsh Industries imekuwa ikinunua mazao yetu mara kwa mara, inatupa hamasa na usimamizi mzuri na hivyo kutuwezesha kuzalisha kwa ubora” anasema Mashaka.
Salome Mgeveke wa Iringa anasema pilipili za Mwendokasi zimemsaidia kupata uhakika wa fedha ili aweze kusomesha na kuwahudumia watoto wake wawili waliotelekezwa na baba yao.
"Inachukua kati ya miezi mitatu hadi mitano tangu kupanda hadi kuvuna kama mazao ikiwa yatatunzwa ipasavyo," anasema.
Mama huyo anasema hana wasiwasi tena ni wapi atapata ada ya mapacha wake kwa sababu pilipili ya Mwendokasi inamsaidia kukidhi mahitaji yake ya sasa.
Darsh Industries, ambayo pia hutengeneza bidhaa nyingine zinazotokana na usindikaji wa matunda na mboga mboga imekuwa ikifanya kazi na shirika la Uholanzi la Rijk Zwaan, kutoa ushauri na mbegu bora kwa wakulima ili kukuza kilimo cha pilipili nchini kote.
Darsh Industries imekuwa ikichakata Mwendokasi kwa njia ya kisasa na baadaye kuifunga kwa ufanisi, ili kuhakikisha mtumiaji anaweza kupata bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.
Wachuuzi wa mitaani na wafanyabiashara wadogo wakiwemo wauza chipsi na mihogo wanaeleza kuwa pilipili Mwendokasi umeleta maendeleo makubwa ndani ya biashara zao.
Jamal Hoza, ambaye ni muuza chipsi kutoka Temeke jijini Dar es Salaam, anasema kuwa ubora wa mchuzi wa Mwendokasi umemsaidia kuongeza mauzo na kuongeza sifa yake kwa wateja wake.