MAMBO kwa kiungo fundi wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ yanazidi kunoga, kwani wakati mashabiki wakiamini jamaa huenda akarudi kambini, lakini jamaa juzi jioni alisepa zake kimyakimya na kutinga Zanzibar na huko kwa sasa anaishi kishua zaidi.
Achana na jana asubuhi kuichezea timu yake ya zamani ya JKU katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege na kuinusuru isipoteze mechi kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung, lakini Fei kwa sasa maisha yake yamebadilika ikiwamo kuwa na ulinzi unaomlinda kama mastaa wa Bongofleva.
Awali, kulikuwa na taarifa kwamba Fei alishamalizana na viongozi wa klabu ya Yanga iliyodaiwa imewatumia vigogo kuzungumza naye ili arudi kambini, lakini ukweli hizo zote zilikuwa ni porojo kwani jamaa alishatimkia Zanzibar na jana alivaa uzi mwekundu wa JKU na kucheza na Mlandege na kuwasaidia mabingwa hao wa zamani wa Zanzibar kushinda mechi hiyo ya kirafiki kwa mabao 5-1.
Hata hivyo, habari kutoka kwa watu wa karibu wa kiungo huyo wa timu ya taifa, wamebainisha kwamba Fei ana ulinzi mkali na pia anatembelea gari lenye vioo vyeusi (tinted) tofauti na alivyokuwa akiitumikia Yanga, ambako alikuwa akiishi simpo akitumia usafiri wa pikipiki jamii ya Vespa.
Tangu kuibuka kwa sakata la kuvunja mkataba na Yanga ili awe huru akihusishwa na klabu ya Azam, Fei alipokuwa Dar alikuwa sio mtu wa kuzurura kutokana na muda mwingi kujichimbia ndani.
Pia inaelezwa hata alipokuwa anataka kutembea basi kile ambacho anakitaka aliletewa moja kwa moja katika nyumba moja ya hapa jijini aliyokuwa anakaa tofauti na kwake na ndipo ikavuma kuwa anataka kuondoka nchini kwenda mapumziko ughaibuni, lakini ghafla akaibukia Zenji.
Hakuna anayejua Fei aliondoka Dar kwa kutumia usafiri wa boti ama ndege kwani ilikuwa na usiri mkubwa kabla ya asubuhi ya jana kuibukia katika mazoezi ya JKU na kuungana na wachezaji wa timu hiyo ya Ligi Kuu ya Zanzibar, lakini kubwa ni kubadilisha maisha aliyozoeleka kuishi visiwani humo.
Mmoja wa watu wa karibu na Fei aliliambia Mwanaspoti kwamba mchezaji huyo amebadilika kwa kiasi kikubwa kwa sababu hapendi kujionyesha.
“Fei alikuwa akija likizo tunakuwa naye sana, lakini kwa sasa kiukweli hapendi kuonekana kabisa, hata tukiwa tunaenda kula urojo hashuki kwenye gari kabisa yaani, yule muuzaji anatuletea garini,” alisema na kuongeza;
“Kiukweli yaani sidhani kama Fei anarudi tena Yanga kwa namna ambavyo tumezungumza na inaonekana ana watu wanamlinda sana.”
MAKOCHA WAMTETEA
Wakati wadau hasa mashabiki wa Yanga wakiendelea kumkomalia Fei na kuona kama ameisaliti klabu hiyo, makocha wa klabu za visiwani Zanzibar wamemtetea katika uamuzi wake wa kutaka kuondoka Yanga wakidai kilichomfanya afanye hivyo ni masilahi tu.
Kocha wa JKU, Sheha Khamis, aliyemtumia jana baada ya kuwaibukia mazoezini na kucheza mechi hiyo ya kirafiki, alisema ni kawaida ya Fei anapokuwa Zanzibar kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya kufanya mazoezi, hivyo haikumshitua baada ya kumuona licha ya kuwepo sekeseke lake na Yanga.
Alisema anachokiona kwa Fei kwenye ishu yake na Yanga ni maslahi yake kwani anajua soka ni la muda mfupi, hivyo anapokuwa kwenye kiwango anatamani kutengeneza maisha yake.
“Kwanza yupo sawa, hana presha yoyote kama ilivyo mtandaoni ambapo mashabiki wanasema mengi, halafu anaipenda Yanga, kinachomsumbua ni wakati huu ambapo ana nguvu na yupo kwenye kiwango haoni maslahi yanayomstahili.
“Sababu kubwa ya kutaka kuondoka anataka jasho lake liende kihalali, pia anajua wanaomshangilia leo, kesho atakapokuwa na maisha magumu watamzomea, hilo ndilo analoliwaza zaidi tofauti na wanavyomchukulia baadhi ya watu ambao hawajajua ukweli wa mambo na hawajakaa naye akawaeleza.
“Ninachowashauri Yanga kama wazazi wangekaa naye chini na siyo kutumia nguvu nyingi kwenye mitandao ya kijamii, pia wakumbuke Fei huyohuyo ndiye alikuwa nao nyakati za dhiki kwa nini wanapopata hawaoni hilo.”
Kwa upande wa Kocha wa Mlandege, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ alisema Fei Toto ni kijana wao, hivyo wanampokea kwa mikono miwili katika timu yoyote.