UNICEF ikisaidia familia za watoto wenye ulemavu kuhudhuria shule katika wilaya maskini zaidi za Maputo na Matola nchini Msumbiji.

3 Disemba 2022 Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu duniani, na kwa mwaka huu inaangazia mchango wa ubunifu katika kuchochea ulimwengu wenye usawa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa siku hii amesema ulimwengu unakabiliwa na msururu wa majanga ambayo yanaathiri watu wenye ulemavu hivyo kunahitajika kupatikane suluhu za mageuzi ili kuwezesha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs na kutomwacha mtu yeyote nyuma.

Taarifa ya ujumbe wake huo iliyotolewa jijini New York Marekani imemnukuu Guterres akisema suala la mageuzi linahitaji ushirikiano mkubwa wa sekta ya umma na binafsi ili kuandaa mikakati ya pamoja kwakushirikiana na watu wenye ulemavu.

“Msingi wa ushirikiano huu lazima uwe na ushirikishwaji kamili wa watu wenye ulemavu ili uweze kujumisha utofauti wao katika michakato yote ya kufanya maamuzi. Ubunifu na teknolojia zinaweza kuwa zana zenye nguvu za kuwajumuisha” amesema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Guterres ameeleza kuwa watu wenye ulemavu wakijumuishwa wanaweza kuongeza ufikiaji wa habari, elimu, na kujifunza maisha yote. Na wanaweza kufungua maeneo mengine mapya kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika nguvu kazi na jamii kwa ujumla na kwa usawa.

“Lakini ili tuweze kufikia hili la kutumia vyema teknolojia, ni lazima kwanza tuondoe mgawanyiko wa kidijitali na kulinda haki za binadamu katika anga ya kidijitali. Kwa upande wetu, Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Kujumuisha Watu wenye Ulemavu unatoa ramani halisi ya kuendeleza ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu na kuwafikia katika kazi zote za Shirika hili. Amesema Guterres na kuongeza kuwa “Tunafanya haya kuanzia makao makuu hadi mashinani, tunafanya kazi kutathmini, kushughulikia na kukuza ufikiwaji wa kidijitali na tunaongoza kuwa mfano wa ujumuishaji wa watu wenye walemavu.”

Guterres amehitimisha ujumbe wake kwa kusema katika siku hii na kila siku, hebu tushirikiane katika kutafuta suluhisho bunifu ili kujenga ulimwengu unaofikiwa na wenye usawa kwa wote.