Kashfa mkopo wa siri wa Sh6.2 trilioni

2 miezi imepita 28

Jumamosi, Desemba 03, 2022

By  Mwandishi Wetu

Mwananchi Digital

Mwananchi

Muktasari:

 Mahakama maalumu nchini Msumbiji imeanza kutoa hukumu ya kesi ya ‘mikopo ya siri’ ya dola za Marekani zaidi ya 2 bilioni inayomhusisha Rais wa sasa, Filipe Nyusi na mtoto wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Armando Guebuza.

Maputo. Mahakama maalumu nchini Msumbiji imeanza kutoa hukumu ya kesi ya ‘mikopo ya siri’ ya dola za Marekani zaidi ya 2 bilioni inayomhusisha Rais wa sasa, Filipe Nyusi na mtoto wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Armando Guebuza.

Serikali ya Msumbiji ilipata mikopo ya siri kati ya dola za Marekani zaidi ya 2 bilioni (zaidi ya Sh4.6 trilioni) na dola 2.7 bilioni (zaidi ya Sh6.21 trilioni) mwaka wa 2013 na 2014 kutoka benki za kimataifa ili kununua meli za uvuvi na meli za uchunguzi.

Hata hivyo, mikopo hiyo ambayo haikutolewa taarifa bungeni wala kwa wananchi iligundulika mwaka 2016.

Wakati kashfa ya madeni ya siri ilipoibuka, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na wafadhili wengine walisitisha misaada ya kifedha na kusababisha thamani ya sarafu ya nchi hiyo kuporomoka.

Mtoto wa Guebuza, Ndambi Guebuza ni miongoni mwa watuhumiwa 19 walio mahabusu wakisubiri hukumu hiyo.

Pia, Waziri wa Fedha, Manuel Chang aliyesaini mikopo hiyo anashikiliwa nchini Afrika Kusini tangu mwaka 2018 akisubiri utaratibu wa kupelekwa Marekani kwa tuhuma za kutumia mfumo wa fedha wa Marekani kutenda ulaghai huo.

Juzi, Jaji Efigenio Baptista wa mahakama maalumu iliyoundwa katika gereza lenye ulinzi mkali jijini Maputo, alisema hukumu ya kesi hiyo yenye kurasa 1,388 itachuka siku tano kusomwa.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mahakamani hapo Agosti mwaka jana hadi Machi mwaka huu na Rais wa zamani Guebuza alikuwa mmoja wa mashahidi katika kesi hiyo.

Rais Nyusi anatajwa kuhusika kwenye kashfa hiyo kwa kuwa wakati mikopo hiyo ya siri inachukuliwa yeye alikuwa Waziri wa Ulinzi, huku jeshi likitajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa na miradi iliyokopewa fedha hizo.

Watuhumiwa wote 19 wamekana mashtaka ya usaliti, utakatishaji wa fedha na rushwa.

Kashfa yenyewe

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, kampuni tatu kwa siri zilichukua mkopo wa dola za Marekani zaidi ya bilioni mbili hadi 2.7 bilioni kwa dhamana ya Serikali.

Fedha za mikopo hiyo zililipwa kati ya mwaka 2012 na mwaka 2013 kwa ajili ya kununua meli za uvuvi na meli za uchunguzi, mradi ambao ulikuwa ukifanywa na kampuni za kigeni.

Bunge la Msumbiji ambalo ndilo lilitakiwa kutoa idhini ya mkopo huo halikuhusishwa na kwamba katika mradi wa jeshi uliotakiwa kuendelezwa, hakuna kilichofanyika.

Nyusi ahusishwa

Rais wa sasa wa Msumbiji ni miongoni mwa wanaohusishwa na kashfa hiyo pamoja na viongozi wengine wa Serikali na wale chama tawala cha Frelimo.

Taarifa zinadai Nyusi akiwa Waziri wa Ulinzi alifahamu mradi huo, lakini mwenyewe alikana tuhuma hizo.

Wakitoa ushihidi wao mahakamani, mmoja wa viongozi wa zamani na mshauri wa idara ya usalama, Cipriano Mutota na mfanyakazi wa zamani wa ubalozi wa Uingereza mjini Maputo, Teoflo Nhangumele, walidai Nyusi alikuwa mmoja wa wahusika muhimu kwenye mpango huo.

Hata hivyo, jina la Nyusi halikutajwa mahakamani hapo na kilichotajwa ni waziri wa zamani wa ulinzi.

Ukopaji wenyewe

Msumbiji, iliyo miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, ilichukua mikopo hiyo bila kulishirikisha Bunge la nchi hiyo.

Deni lilifichwa lakini hatimaye likafichuka mwaka 2016 na kusababisha wafadhili kama IMF kuondoa misaada ya kifedha nchini humo.

Baadaye ukaguzi huru ulifanyika ikabainika dola 500 milioni zimetumika kinyume cha utaratibu na hazijulikani zilipo.

Rais wa zamani wa Msumbiji, Armando Guebuza alikuwa shahidi wa ngazi ya juu zaidi katika kashfa hiyo. Alikuwa Rais wa Msumbiji kuanzia mwaka 2005 hadi 2015.

Mwanawe mkubwa, Ndambi Guebuza ni miongoni mwa washtakiwa 19 wanaokabiliwa na mashtaka hayo.

Ndambi alikamatwa Februari 2019 na amekuwa mahabusu tangu wakati huo.

Hata hivyo, Ndambi alikana mashtaka ya kupokea rushwa ili kumshawishi baba yake aidhinishe mpango wa kufanikisha mkopo huo wa siri.

Ndambi ni mtoto wa kwanza kati ya wanne wa Rais Guebuza. Alikamatwa akiwa nyumbani kwake kuhusu mtandao wa rushwa aliotumia kwa kuchukua “deni la siri” la taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Fedha hizo zilielezwa zinawezesha kununua meli, vyombo mbalimbali vya kusafiria na meli za kijeshi.

Endapo Msumbiji italazimika kulipa mikopo hiyo, kuna riba ya zaidi dola 4 bilioni, suala litakalosababisha hali mbaya ya kiuchumi, ikiwamo kupungua kwa huduma za jamii, taasisi na kukosa fedha za maendeleo kwa ujumla.

IMF yarejesha misaada

Hivi karibuni, IMF ilitia saini mkopo wa dola milioni 456 kwa ajili ya Serikali ya Msumbiji, ikiwa ni msaada wa kwanza wa aina hiyo kutolewa tangu kashfa ya madeni ya siri kuibuka miaka sita iliyopita.

Source : Mwananchi

SHARE THIS POST