Kigogo TFF ataja tatizo la waamuzi Ligi Kuu

1 mwezi umepita 39

By  Imani Makongoro

[email protected]

Mwananchi Communications Limited

Wakati mwamuzi Hans Mabena akipelekwa kwenye  kamati ya waamuzi kwa kushindwa kumudu mchezo kati ya Azam na Tanzania Prisons iliyochezwa kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, aliyewahi kuwa katibu mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa ametaja mambo manne yanayochangia 'kuboronga' kwa baadhi ya waamuzi.

Pia ameshauri kuwe na utaratibu wa kulea waamuzi vijana na kuwajengea uwezo zaidi ili kuwatumia na kupunguza malalamiko kwa waamuzi wengi kushindwa kumudu mchezo kwenye Ligi nchini.

"Nakumbuka nikiwa TFF kulikuwa na programu kama hiyo kwa vijana chini ya miaka 17, ilisaidia.

"Haya malalamiko ya waamuzi wengi kipindi hiki kinachangizwa na mambo mengi, inawezekana ni uwezo mdogo wa kutafsiri sheria au wanakosa utimamu wa mwili ili kuwa eneo la tukio kwa wakati muafaka.

"Au wanaukosa kujiamini na kushindwa kufanya uamuzi, lakini kingine kinacho ongeza malalamiko ni mechi kuonyeshwa laivu, kwenye televisheni kuna vitu vinaonekana ambavyo kwa macho ya binadamu hawezi kukiona," amesema Mwesigwa.

Jana kamati ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)  ilieleza kumpeleka Mabena kwenye kamati ya waamuzi ya TFF kwa kushindwa kuumudu mchezo wa Azam na Prisons.

Mabena anaingia kwenye orodha ya waamuzi waliopelekwa kwenye kamati hiyo kwa hatua zaidi huku  mkufunzi wa waamuzi, Lesley Liunda katika moja ya mahojiano na Mwananchi Digital alikaririwa akisema adhabu sahihi kwa mwamuzi aliyeharibu mchezo ni kumshusha daraja.

"Hii itasaidia kuongeza umakini, lakini si kumfungia kwa kuwa ukimfungia unampotezea dira, ila ukimshusha daraja na yule anayefanya vizuri unampandisha kuchezesha ligi ya juu, itaongeza umakini," alisema Liunda.

Hata hivyo, Mwesigwa ametaja njia nyingine ya kupata waamuzi bora ni kuwa na programu ya waamuzi vijana chini ya miaka 17 na kuanza kuwajenga kuanzia chini.

"Tuwe na programu ya kuwanoa kwa muda mrefu na kuanzia chini, kuliko kuanza nao wakiwa wakubwa, wakianza profesheno katika levo ya chini ya miaka 17 tunaweza kutengeneza aina ya waamuzi mahiri zaidi na wakafika mbali," amesema.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST