Mgunda atoa onyo

3 miezi imepita 38

By  Clezencia Tryphone

Mwananchi Communications Limited

KITENDO cha kikosi cha Wekundu wa Msimbazi Simba kupoteza pointi mbili Kanda ya Ziwa kimemfanya kocha mkuu Juma Mgunda kuongeza nguvu zaidi kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Tanzania Prisons.

Katika mechi za Kanda ya Ziwa, Simba iliifunga Geita Gold mabao 5-0, KMC 3-1 na kuangusha pointi mbili katika sare ya 1-1 dhidi ya Kagera Sugar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema ameyasahau yaliyopita na sasa anatazama michezo inayokuja kuanzia wa Prisons leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mgunda alisema, kwa sasa ameanza kufanyia kazi udhaifu wa kiufundi aliouona katika michezo iliyopita licha ya kupata matokeo chanya ili waendelee kufanya vizuri zaidi.

“Sasa hivi kila timu inajitahidi kuhakikisha inapata matokeo chanya katika kila mchezo ambao inacheza, na sisi Simba malengo yetu ni hayo hayo, ikitokea tukapoteza pointi ni sehemu ya mchezo lakini sio lengo,” alisema Mgunda.

Aidha, Mgunda jana wakati wa mazoezi aliwataka wachezaji wake kuwa watulivu na kuwaheshimu wapinzani wao muda wote wa mchezo.

“Kitendo cha kumuheshimu mpinzani bila ya kujali upo nyumbani au ugenini ni moja ya silaha za ushindi, nina imani kubwa na wachezaji wangu lakini pia nawaheshimu Prisons sio timu ya kubeza,” alisema Mgunda.

Katika msimamo wa ligi hiyo inayoelekea ukingoni Simba inashika nafasi ya pili baada ya kujitupa uwanjani mara 18 ikiwa na pointi 41 huku Prisons ikishika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 21, zote zikiwa nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 47.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST