Mshtakiwa adai kukiri kuua kwa kuogopa kuingizwa spoku

1 mwezi umepita 50

Ally alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aloyce Minde wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa utetezi wake katika kesi ya mauaji inayomkabili, anayotuhumiwa kumuua Maluni, Juni 12, 2014.

Alidai kuwa, Februari 9, 2022 majira ya asubuhi akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi cha Msimbazi, alikwenda afande Apolinary na askari wengine watatu, mmoja kati yao alikuwa wakike.

Alidai walifungua mlango wakamueleza kuwa maelezo aliyoyatoa Februari 8, 2015 mbele ya wakili wake, Juma Mtatiro, hawayataki na kudai wanataka maelezo wanayoyataka wao.

Mshtakiwa huyo akiongozwa na wakili wake, Caroline Kigembe, alidai kama wanataka atoe maelezo upya basi wampigie wakili wake, lakini hawakumpigia na wakamueleza akiri kitu ambacho yeye hakifahamu.

Ally alidai askari wa kike alimshika sehemu zake za siri za mbele, huku mkono wake mwingine ukiwa umeshika spoku ya baiskeli, ikabidi amuulize vipi spoku na sehemu zake za siri? Akamjibu kwani yeye hataki kumuingilia mwanamke?

"Kwa sababu nilimuona mtu mmoja akiwa mahabusu ana vuja damu sehemu zake za siri, nilihofia kuwa na mimi nitakuwa kama yule, niliwaambia nitaandika kama wanavyotaka wao kuliko kuingiziwa spoku," alidai Ally.

Alidai kwa wakati huo tayari walishaandika maelezo yao na afande Apolinary (marehemu) alikuwa nayo mfukoni, na kwamba alisaini maelezo hayo na baada ya hapo walimrudisha mahabusu na kumfungia milango wakaondoka.

Baada ya nusu saa, Ally alidai alikwenda afande Chenga, Apolinary pamoja na askari wengine hawafahamu wakamfunga kitambaa usoni wakamuweka ndani ya gari, walipomfungua kitambaa alijikuta kwenye nyumba ambayo alishapanga huko Ilala Sharif Shamba, Dar es Salaam.

Alidai kuwa hakujua chochote na hakuambiwa jambo lolote akafungiwa kwenye chumba kimoja na ilipofika majira ya saa 10 au 11 jioni wakamtoa ndani wakamrudisha kwenye gari.

Pia, kuhusu mapazia 23 yaliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo, alidai hayo sio muhimu na kwamba yametengenezwa maalum kwa ajili yake ikiwezekana mahakama imrudishie mwenyewe kwa sababu yalipokutwa yeye haishi huko.

Ally alidai kuwa swali la kujiuliza ni kwamba hayo mabaki yaliyokutwa kwenye nyumba ambayo alishawahi kuwa mpangaji, je! Ni kweli ni ya Farihani? Jibu ni kwamba sio kweli kutokana na ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mshtakiwa alitoa swali hilo, kwa sababu Mkemia Mwandamizi kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kaijunga Brassy, wakati anatoa ushahidi kwenye kesi hiyo alidai mabaki ya marehemu Farihani ikiwamo mifupa haikuonesha majibu ya vinasaba (DNA).

Mshtakiwa huyo aliomba mahakama imuachie huru kwa sababu yupo gerezani miaka minane na pia yeye sio muuaji wala hakuwahi kuua na anaomba Mungu amuepushe kwa hilo, anaomba mahakama imuachie huru.

Wakati akijibu swali la Wakili wa Serikali, Aziza Mhina, Ally alidai kuwa Julai 12, 2014 ilimkuta akiwa mahabusu,  tarehe anayotuhumiwa kuwa alimuua Maluni.

Ilidaiwa Juni 12, 2014 mshtakiwa Hemed Ally eneo la Sharif Shamba anatuhumiwa kumuua Farihani Maluni.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST