PM: Idadi watalii yaongezeka hadi 992,690

1 mwezi umepita 30

Alisema, mbali na kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini, pia mapato yatokanayo kutoka sekta hiyo yameongezeka kwa asilimia 81.8 kutoka Dola za Marekani milioni 714.59 mwaka 2020 na kufikia Dola bilioni 1.3 mwaka 2021.

Aliyasema hayo jana alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye ufunguzi wa mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani - Kamisheni ya Afrika unaofanyika jijini Arusha.

“Pia takwimu za mwaka 2022 zinaonesha kuwa Sekta ya Utalii inazidi kuimarika zaidi hususan baada ya uzinduzi wa Programu Maalumu iliyotekelezwa na Rais Samia ya The Royal Tour, iliyozinduliwa rasmi Aprili 2022 katika soko letu la utalii la kimkakati nchini Marekani.”

Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya mwongozo mzuri uliotolewa na Shirika la Utalii Duniani kwa nchi wanachama ikiwamo Tanzania katika kukabiliana na athari za UVIKO - 19. “Kwa msingi huo, ninatumia fursa hii kulishukuru Shirika la Utalii Duniani hususan, kwako Mheshimiwa Zurab Pololikashvili, Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani kwa kuiongoza vyema sekta ya utalii katika kipindi chote cha janga hilo.”

Hata hivyo, alisema lengo la serikali ni kuendelea kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini hadi kufikia milioni tano na mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025. “Utajiri wa vivutio vya utalii tulivyonavyo umeifanya sekta ya utalii kuwa muhimili muhimu wa uchumi wa nchi yetu.”

Kadhalika, Majaliwa alitoa rai kwa mashirika na taasisi za kimataifa kuendelea kuiamini Tanzania na kuichagua kama sehemu sahihi ya kufanyia matukio yenu mbalimbali ikiwamo mikutano adhimu kama huo.

Naye, Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii Duniani, Zurab Pololikashvili, alisema baada ya mlipuko wa janga la UVIKO-19 nchi nyingi duniani ziliathirika kwa kiasi kikubwa katika sekta ya utalii, watahakikisha wanaendelea kuweka mikakati ya kurejesha katika hali yake ya kawaida.

“Wiki iliyopita tulisherehekea siku ya utalii duniani iliyokuwa na kaulimbiu ya Rethinking Tourism, ambayo tunaamini itasaidia kuirejesha sekta hiyo katika hali yake ya kawaida na kuendelea kusaidia kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi na kuongeza idadi ya ajira.”

Alisema, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zina vivutio bora vya kutembelea kwa ajili ya utalii na watu wengi duniani wameitambua kupitia filamu maarufu ya The Royal Tour. “Ninafurahi sana kuwa miongoni mwa watu walioshuhudia filamu hiyo ambayo imenimeweza kuona tamaduni na vivutio vilivyopo katika ardhi hii ya Uhuru na Umoja.”

Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana alisema kuchaguliwa kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya nchi yetu pamoja na jumuiya ya Kimataifa katika masuala mbalimbali yakiwamo ya utalii. Mkutano huo umehudhuriwa na washiriki kutoka nchi 33 wanachama wa Shirika la Utalii Duniani-Kamisheni ya Afrika.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST