Prof. Mkenda ataka ufundishaji somo la maendeleo vyuoni

2 miezi imepita 38

Akizungumza leo Desemba 02,2022 Jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Waziri Mkenda  amesema kuwa  ufundishaji wa somo hilo  uwezeshe wanafunzi hao kufanya tafukuri tundulizi.

Waziri  pia ametaka ufundishaji huo  uwawezeshe wanafunzi  kupata fursa ya  kuchambua historia ya uchumi wa nchi ili kutambua vipindi mbalimbali ambavyo nchi imepitia na tunapoelekea kiuchumi.

"Nimefurahi kuona kupitia mkutano huu mnafanya tathimini ya somo la maendeleo ambalo linawawezesha wanafunzi katika fani zote kuwa wadadisi na kuweza kufanya tafakuri," amesema Prof. Mkenda

Kuhusu Mapitio ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, amesema kwa ujumla  yanalenga kuona mwanafunzi akiwa na udadisi, mahiri na mwenye kujiamini katika kufanya kazi aliyosomea anapohitimu.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma ya Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Colman Msoka amesema mkutano huo ni wa pili kufanyika nchini na unalenga kufanya tathimini ya ufundishaji wa somo la maendeleo chuoni hapo.

Dk. Msoka ameongeza kuwa Taasisi hiyo Mwaka 2023 itakuwa inafikisha miaka 50, hivyo wameona ni jambo muhimu kutafakari kwa kuwa katika miaka hiyo  mambo yametokea ikiwemo kuporomoka kwa ujamaa, ulibelali kuongezeka kwa kasi,  utandawazi na kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, vyote vimebadili namna ya kuishi  hivyo umuhimu wa kubadili mbinu za ufundishaji wa somo hilo.

Mkutano huo  unashirikisha wajumbe kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kutoka nchi za Marekani, Afrika Kusini, Ethiopia, India na Nigeria.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST