Rais Samia amestahili udaktari wa heshima

2 miezi imepita 30

Hivyo ndivyo, Rais Samia Suluhu Hassan alitunukiwa shahada ya heshima ya udaktari wa fasihi (Doctor of Letter- Honoris Causa) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Tangu aingie madarakani Machi 19, 2021 Dk. Samia amefanya mambo mengi kwa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo Watanzania wengi wamekuwa wakipongeza. Mambo mengi yalikuwapo yakiwamo manung’uniko ya baadhi ya watu hali iliyofikia mahali mpaka akaambiwa na baadhi ya viongozi wa dini kuwa ana wajibu mkubwa wa kutibu majeraha ya Watanzania.

Katika muda ambao haujafika miaka miwili, hakika ameonyesha nuru ya safari ya Watanzania kusonga mbele kimaendeleo katika nyanja mbalimbali. Kabla ya kutunukiwa shahada hiyo, zilisomwa sifa zilizomstahilisha ambazo alipopewa nafasi ya kuzungumza, alikiri dhahiri kwamba zinamfaa kutunukiwa shahada hiyo licha ya kwamba alisema mwanzoni aliona kama hastahili.

Katika wasifu uliosomwa kuhusu Rais Samia na mambo ambayo yamefanya atunukiwe shahada hiyo ni pamoja na kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na kuleta utengamano na matumaini mapya kwa taifa la Tanzania. Katika hotuba yake ya kwanza kabisa aliyoitoa baada ya kuapishwa, aliwasihi Watanzania kusimama pamoja na kushikamana, kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa.

Pia alisisitiza kuonyeshana upendo, kudumisha amani, kuenzi utu na uzalendo wetu na kwamba umefika wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kuweka nguvu kwa pamoja kuijenga Tanzania mpya.

Mambo hayo ambayo aliyasisitiza na akiwa amekaa madarakani kwa mwaka mmoja na miezi minane, amefanya mambo ambayo yanaonekana yakiwamo kuinua uchumi wa taifa, kujenga uhusiano wa kiuchumi kitaifa, kikanda na kimataifa. Juhudi zake pia zimewezesha upatikanaji wa mabilioni ya fedha za misaada, mikopo na uwekezaji katika miradi mikubwa kama vile barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, elimu na afya.

Pia ameonyesha dhamira ya kweli ya kukuza uchumi wa nchi hasa kwa kuelekeza nguvu kubwa katika sekta ya kilimo ambayo ni mwajiri wa takriban asilimia 70 ya Watanzania. Ili kufanikisha hilo, serikali yake kwa mwaka 2022/23 imeongeza bajeti hadi kufikia Sh. bilioni 954 na kushusha bei ya mbolea kwa asilimia 50.

Sambamba na hiyo, ameweka juhudi kubwa katika kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji na sekta binafsi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje na kukuza sekta binafsi. Juhudi hizo ni pamoja na kupunguza vikwazo katika upatikanaji vibali na leseni za biashara na kurekebisha kodi mbalimbali.

Dk. Samia pia alionyesha dhamira ya kuendeleza sekta ya utalii kwa kushiriki filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” kwa madhumuni ya kutangaza kimataifa vivutio vya utalii nchini Tanzania. Filamu hiyo ambayo imeonyeshwa katika nchi mbalimbali duniani, imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii wanaoitembelea Tanzania ambalo linakadiriwa kufikia asilimia 34 kufikia Juni, mwaka huu.

Katika siasa, ndani ya kipindi kifupi, uongozi wake umeonyesha nia thabiti ya kupanua ushiriki wa vyama vya siasa katika siasa za nchi. Pia utawala wake umepunguza kwa kiasi kikubwa, sintofahamu za kisiasa na kuashiria matumaini mapya ya amani na ushirikiano. Katika azma yake ya kujenga demokrasia na umoja, amechukua hatua za makusudi kuleta maridhiano kati ya vyama vya siasa kwa kuunda Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa.

Pia ameonyesha dhahiri na kusisitiza kwa vitendo umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu katika uongozi ikiwamo kuimarisha usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali na kukemea unyanyasaji na ukatili wa kijinsia. Yako mengi ambayo Dk. Samia ameonyesha katika uongozi wake kuwa amestahili kupata shahada hiyo ya udaktari wa heshima na Watanzania wanapaswa kumpongeza.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST