Saido apewa kazi tatu Simba SC

3 miezi imepita 41

By  Thobias Sebastian

Reporter

Mwananchi Communications Lmited

KWA kiwango alichokionyesha mazoezini, kiungo mpya wa Simba, Saido Ntibazonkiza leo Ijumaa ana nafasi kubwa ya kuanza kikosini wakati timu hiyo ikiikaribisha Tanzania Prisons katika Ligi Kuu Bara.

Simba na Prisons zitaumana kuanzia saa 12:15 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Wekundu wakiwa nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko katika kikosi kwa ajili ya ingizo jipya la Saido aliyesajiliwa kutoka Geita Gold na kufanikiwa kupata vibali.

Badiliko hilo la Saido kikosini linatokana na namna alivyokukiwasha mazoezini huku akikabidhiwa mambo matatu watakapokabiliana na Prisons iliyowekewa Sh 30 milioni kama itashinda mechi hiyo.

Kwa mujibu wa mazoezi hayo, Saido ataanza kikosini atacheza namba 10 nyuma ya mshambuliaji wa mwisho ambaye atakuwa nahodha, John Bocco mwenye mabao sita hadi sasa katika ligi.

Kutokana na mazoezi hayo, Simba itaingia na mfumo wa (4-2-3-1), kwa maana ya mabeki wanne, viungo wakabaji wawili, viungo washambuliaji watatu na hapo ndiyo atakuwemo Saido na mbele yake Bocco.

Kwenye mstari wa wachezaji wanne safu ya Simba wataanza, Saido, Bocco, Clatous Chama mwenye mabao matatu na pasi za mwisho 10 na Augustine Okrah aliyefunga bao lake la tatu msimu huu mchezo uliopita dhidi ya KMC huku akiwa ametoa pasi ya mwisho moja.

Katika mazoezi hayo kuna wakati Kocha, Juma Mgunda alimbadilisha, Okrah na kumuingiza Pape Sakho na huenda hata kwenye mechi na Prisons leo akafanya hivyo pia kulingana na mchezo utakavyokuwa.

Kwenye mazoezi ya Simba, Saido alipewa majukumu matatu maalumu kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji wenzake na hilo aliweza kulifanya vizuri huku, Bocco, Okrah na Chama wakifanya kazi ya kufunga mabao.

Jukumu lingine, Saido ambaye alifanya vizuri akiwa na Yanga alipewa kazi ya kupiga mipira iliyokufa kama faulo zile za nje ya boksi na jukumu la tatu ilikuwa kupiga kona, huku akionekana kulifanya zoezi hilo vizuri kwani makipa wa kikosi hicho walikutana na wakati mgumu.

Saido alionekana kuwa wa moto katika mazoezi hayo alikuwa na maelewano mazuri na wachezaji wenzake kama alikuwapo kwenye timu kwa muda mrefu huku akipewa jukumu la mwisho kufunga mabao kutokana na mashambulizi yanatengenezwa na wachezaji wengine.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST