Serikali yatoa maagizo kwa vyuo vinavyotekeleza mradi HEET

2 miezi imepita 50

Wito huo umetolewa leo Desemba 01, 2022 Jijini Dar es  Salaam   na Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo  Dk. Francis Michael wakati wa utiaji saini wa makubaliano ya ruzuku ya Mradi wa HEET kwa Taasisi za Elimu ya Juu zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Kiongozi huyo amesema mradi huo unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika mawanda ya elimu ya juu nchini kwa kuwaandaa vijana watakaokuwa na uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa kwa kujiajiri ama kuajiriwa.

"Rais Samia Suluhu Hassan na Benki ya Dunia wanataka kuona mradi huu ukiwaondoa vijana barabarani kwa kuwapatia ujuzi, maarifa na stadi zitakazowawezesha kujiajiri ama kuajiriwa, hivyo twendeni tukatekeleze mradi huu kwa mtazamo huo," amesisitiza.

Katibu Mkuu huyo amezitaka taasisi hizo kuhakikisha wanatekeleza mradi huo kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa, huku akisisitiza matumizi makini ya fedha.

Naye, Mratibu wa Mradi huo kwa Wizara ya Fedha  na Mipango Amani  Ngedu ameishukuru Wizara ya Elimu na Benki ya Dunia kwa kuzipatia Taasisi hizo mradi huo kwa kuwa unakuwa mradi wa kwanza mkubwa kwa taasisi hizo.

Ameongeza  kuwa ushirikiano uliopo kati ya Wizara hizo mbili utasaidia katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo katika taasisi hizo kwa ufanisi na weledi.

Taasisi za Elimu zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango zinazonufaika na Mradi huo ni Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Mipango (IRDP), Chuo cha Takwimu (EASTC), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).

Source : Nipashe

SHARE THIS POST