Simba: Tutarudi kileleni Ligi Kuu

2 miezi imepita 27

Hata hivyo, Yanga ambao ni mabingwa watetezi na wana mechi moja ya kiporo, bado wako kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 32, sawa na Azam FC huku Simba yenye pointi 31 ikiwa kwenye nafasi ya tatu.

Endapo Yanga iliyoko chini ya Mtunisia, Nesreddine Nabi, ingepata matokeo mazuri katika mechi hiyo, ingeendelea kuwaacha mbali watani zao, Simba.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia gazeti hili jana, kupoteza kwa watani zao kumekuwa ni faraja kwao na imewarejesha kwenye mbio za kuwania taji hilo ambazo bado ziko wazi.

Ahmed alisema sasa kuna taswira nzuri na kupata mwanga wa kurejea kileleni hasa wachezaji wa wekundu hao wa Msimbazi wakiendelea kujitoa kutafuta matokeo michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopo mbele yao.

Ofisa huyo alisema benchi la ufundi linaendelea kukiandaa vizuri kikosi chao na wanafurahi kuona kila mchezaji wa Simba yuko tayari kupambana na hatimaye kufikia malengo yaliyowekwa na timu hiyo iliyoko kwenye hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alisema wanafahamu na wanatambua mchezo dhidi ya Coastal Union utakuwa mgumu na wenye ushindani, hivyo wamejipanga kucheza kwa nidhamu muda wote.

"Hakuna mechi rahisi msimu huu, tena kwetu sisi kila mchezo ni zaidi ya fainali, tutaingia uwanjani kuwakabili Coastal Union kwa kuwaheshimu, ni wapinzani ambao wako imara na wao dhamira yao ni kupata pointi tatu," alisema Ahmed.

Aliongeza haitakuwa na maana ya kushinda mchezo uliopita ambao uliwapa furaha mashabiki na baada ya kupita siku chache wakapoteza mechi, wakati wanahitaji kujiimarisha kwenye msimamo wa ligi hiyo ya juu nchini.

Alisema kila mchezaji anajua wanakutana na timu yenye wachezaji wazoefu na wanaofahamu vyema falsafa za kocha (Juma Mgunda), ambaye alitoka kwenye kikosi hicho, hivyo kila upande unatakiwa kuongeza utulivu.

"Tunahitaji kupata matokeo chanya katika  mechi ya Coastal Union, haitapendeza kwa sababu matuamini ya sisi kurejea kileleni yamerudi. Tuliwapa furaha baada ya kuifunga Polisi Tanzania, tunataka furaha hiyo iendelee, tunahitaji kuendeleza ushindi huu, tunatakiwa kujituma na kujitoa," aliongeza kiongozi huyo.

Alisema pia taarifa njema ndani ya kikosi chao ni kuimarika afya kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi wakiwamo, Jimmyson Mwanuke na Mohammed Hussein (Zimbwe Jr).

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema kikosi chao kimefika salama Tanga na wanatarajia kuendelea na mazoezi kwa ajili ya kukamilisha kazi iliyowapeleka.

Rweyemamu alisema wanatambua mechi hiyo haitakuwa rahisi kwa sababu Coastal Union walipoteza mchezo uliopita wakiwa kwenye uwanja na hivyo wataingia kurekebisha makosa.

"Kila mechi ni ngumu kwetu, tunajua kila timu inazihitaji pointi ili kujiimarisha, walifungwa mechi iliyopita, haitakuwa rahisi tena kupoteza, watapambana kutafuta pointi lakini pia kuwapa furaha mashabiki wao," alisema Rweyemamu.

Wakati huo huo, Kagera Sugar inatarajia kuikaribisha Ihefu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba wakati Singida Big Stars itawaalika Namungo FC kutoka mkoani Lindi.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST