Simba yafunguka inachokitaka CAF

1 mwezi umepita 31

Primeiro de Agosto inatarajia kuikaribisha Simba katika mechi ya kwanza ya hatua ya kwanza itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Estadio 11 de Novembro mjini Luanda.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema jana wamejipanga kucheza kwa tahadhari kwa sababu wanafahamu ubora wa wapinzani wao na rekodi nzuri waliyonayo walipokutana mara ya mwisho.

Ahmed alisema wanafahamu mechi hiyo haitakuwa rahisi kama baadhi ya watu wanavyodhani kutokana na wapinzani wao kuwa na kikosi bora, ambacho kinatarajiwa kuwapa ushindi.

Alisema Simba haitabweteka katika mechi hiyo ya kwanza na ile ya marudiano itakayochezwa Oktoba 16, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

"Tumeshapeleka mtu Angola kwa ajili ya maandalizi ya awali, ameshafanya kila kitu, tunajua wapi tutafikia, wapi tutafanya mazoezi, hii ni kuonyesha ni namna gani tuko makini na tuna dhamira ya kutinga hatua ya makundi.

Hatuichukulii poa hata kidogo timu hiyo kwa sababu tunafahamu ubora wao, msidhani kama tunawadharau wapinzani wetu, wao pia kama sisi wana dhamira ya kutaka kutinga hatua ya makundi," alisema Ahmed.

Ofisa huyo aliongeza malengo ya Simba msimu huu ni kufika robo fainali au kwenda mbele zaidi kwa sababu uwezo wa kufika hatua hiyo wanao.

"Tukifika robo fainali tutakuwa hatujafeli ila tutakuwa tumeishi pale tu ambapo tumeishia msimu uliopita. Tukitolewa hatua hii, au tukaingia makundi na kushindwa kuvuka, tutakuwa tumeshindwa, tena kwa kiasi kikubwa, kitu ambacho hatutaki kukipa nafasi kwenye klabu yetu kwa sasa," alisema Ahmed.

Aliongeza kwa sasa Kaimu Kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda, yuko katika harakati za kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya mechi hiyo na ile ya marudiano ili kufikia malengo.

"Mpira wa kisasa ni mbinu, morali, na kujiamini ukiwa na kitu hicho kwenye timu yako unaweza kupata ushindi sehemu yoyote ile, tunamshukuru kocha Mgunda kwa sababu amekuwa ni zaidi ya kocha, ni kocha, mlezi na mwanasaikolojia, anaweza kulea wachezaji, hata akikata tamaa ana namna ya kuzungumza nao kama baba, pia anaweza kucheza na saikolojia ya wachezaji, amewabadilisha wachezaji kwa sababu wamekuwa wakipambana uwanjani, wana morali na kujiamini kumeongezeka chini yake," Ahmed alisema.

Naye Mgunda aliliambia gazeti hili hana hofu na wachezaji wake kwa sababu wanafahamu wanachotakiwa kukifanya katika mechi zote mbili.

Mgunda alisema licha ya timu yake kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji, bado analazimika kurekebisha makosa yaliyojitokeza na hilo ni jambo la kawaida katika mchezo wa soka.

"Tunakabiliwa na dakika 180 ngumu za ugenini na nyumbani, katika soka hakuna mechi rahisi, sisi tunajipanga na wenzetu pia wanajipanga, ili kuona tunapata matokeo chanya, tunaendelea kujiimarisha kwa kufanyia kazi mapungufu yetu," alisema Mgunda.

Katika mchezo huo wa Jumapili, Simba itaendelea kukosa huduma ya beki wake, Shomari Kapombe, Peter Banda na Jimmyson Mwanuke ambao ni majeruhi.

Kabla ya kurudiana na Waangola hao, Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara itawafuata Singida Big Stars katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa Oktoba 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Liti ulioko mkoani Singida.

Simba inatarajia kuelekea Luanda, Angola na baada ya mechi itaondoka siku hiyo hiyo kwa ndege ya kukodi kurejea nyumbani kuwasubiri Waangola hao.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST