Simba yajiandaa kushusha jembe

1 mwezi umepita 53

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' alisema mpango mkakati umeshaanza ili kuhakikisha nafasi hiyo inazibwa na mchezaji wa daraja la juu kwa kushirikiana na benchi la ufundi.

Salim alisema kwa sasa wapo katika  mazungumzo na wawakilishi wa Dejan na yatakapokamilika wataweka wazi, lakini kwa sasa wataendelea kuwaamini wachezaji wa nafasi hiyo waliokuwa nao.

"Jambo muhimu ni kuona nafasi hiyo inazibwa na straika mwenye uwezo mkubwa wa kufumania nyavu, lakini mchakato huu tunashirikiana na benchi la ufundi, sisi wenyewe umuhimu tunauona, tunalisikiliza benchi la ufundi linahitaji kitu gani, lakini kwetu sisi mpango mkakati umeshaanza mara moja kuhakikisha nafasi hiyo inazibwa na siku zote, Simba huwa hatufanyi makosa kwenye jambo hilo ni suala la wakati tu. Sina shaka Wanasimba watafurahi na kile ambacho wanakitarajia, huenda ukawa ndiyo wakati wake umefika," alisema bosi huyo.

Ingawa bosi huyo hakumtaja mchezaji ambaye watamsajili, lakini zipo habari zinasema tayari klabu hiyo ilishampa mkataba wa awali Cesar Mandoki ambaye wakati huo alikuwa akiichezea Vipers ya Uganda.

Usajili wa Manzoki katika dirisha dogo la usajili uliingia changamoto kutoka katika Vipers ambaye sasa anaichezea Dalian Professional ya China kwa mkataba wa muda mfupi.

Kuhusu Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, mwenyekiti huyo alisema walifanya uamuzi sahihi, akiongeza hata kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wakati wamewasilisha jina la kocha huyo ili kulipitisha hakukuwa na mjumbe yeyote aliyepinga.

"Tulikuwa wajumbe saba, wote tulikubali jina lilipowasilishwa, na hata tulipompigia simu na yeye (Mgunda), wala hakuchukua muda kukubali, kwa hiyo hatukumpata kwa bahati. Kwa sasa ndiyo Kaimu Kocha Mkuu, kama kuna kocha mpya atakuja, au ataendelea yeye, tuvute subira," alisema bosi huyo.

Aliongeza wanaamini Mgunda ataisaidia Simba kufikia malengo yao katika mashindano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo msimu uliopita walivuliwa ubingwa.

"Tunapambana katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri, lengo letu ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika mashindano yote tunayoshiriki, tunajua mashabiki wetu wanahitaji furaha, hicho ndio tunachokitarajia sisi viongozi pia," Salim aliongeza.

Kikosi cha Simba kinatarajia kuondoka nchini kesho kuelekea Angola kuwafuata Primiero De Agosti katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa keshokutwa.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST