TPSF IKITAMBA KUNG’ARA...

2 miezi imepita 43

TPSD22 imeandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na wadau muhimu wa sekta binafsi na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, kuenzi na kutambua mchango wa sekta binafsi katika uchumi wa nchi.

Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula, anasema zaidi ya wajumbe 1,000 ambao ni viongozi wa kisekta, wakurugenzi watendaji na maofisa waandamizi wa serikali watakusanyika kujadili dhima kuu ya ‘Kuimarisha Ushindani wa Sekta Binafsi.’

“Lengo la tukio hili ni kutathmini mafanikio ya sekta binafsi kipindi cha 2021-2022, huku tukiangazia mazingira bora ya biashara na uwekezaji ambayo yamechochea ukuaji wa uchumi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita," anasema Ngalula.

Aidha, anabainisha kuwa ongezeko la biashara na Kenya kwa asilimia 95, limechangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania na mwenyekiti huyo anasema, mafanikio mengine muhimu ya sekta binafsi ni pamoja na ukuaji shughuli za uwekezaji, kupanuka wigo wa ajira, kodi, na bidhaa za Tanzania kufikia masoko mapya.

“Maadhimisho haya yatatumika kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo. Tunatakiwa kuueleza ulimwengu fursa za uwekezaji zinazopatikana Tanzania,” anasisitiza Ngalula.

Aidha, anasema kilimo ni sekta yenye kuleta faida kubwa kwa watu wenye nia ya kuwekeza, akifafanua: “Hivi karibuni tumesaini mikataba muhimu ambayo imepelekea mazao kutoka Tanzania kuuzwa nchi za nje.

“Kwa mfano, China imeagiza zaidi ya tani 40,000 za maparachichi kutoka Tanzania. Tumeshuhudia makubaliano kama haya yakifanyika baina yetu na Afrika Kusini na India.”.

Kupitia Sera ya Diplomasia ya Uchumi, Ngalula anasema fursa za uwekezaji kwenye sekta ya madini zinatangazwa nje ya nchi na matokeo yake sasa yanaonekana.

Anasema mwaka 2021, serikali ilisaini mikataba minne na kampuni ya uchimbaji madini yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 735; na kwamba mikataba hiyo ina thamani kubwa zaidi nchini Tanzania.

Mwenyekiti huyo anafafanua kuwa, kiwango cha ukuaji uchumi baada ya janga la UVIKO-19 kinatakiwa kuwa endelevu ikikua na  akisema hivi sasa nchini, uchumi unakua kwa kasi asilimia 5.1.

“Sekta binafsi imekuwa sehemu ya kutoa suluhisho kwa changamoto za uchumi kupitia biashara ndogo na za kati ambazo ni chanzo cha kipato kwa familia na uchumi wa taifa,” anasema na kuongeza:

“Familia nyingi Tanzania zinategemea biashara ndogo na za kati; kwa mujibu wa Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agriculture (TCCIA), takribani asilimia 35 ya pato la taifa linatokana na kundi hili. Maongezi yetu (yanayoanza sasa yatajikita katika nafasi ya sekta binafsi kwenye kuisaidia nchi kufikia dira yake ya maendeleo.”

Pia, ni uzinduzi utakaoendana na makongamano ya kikanda ya wauzaji na wanunuzi yaani  kitaalamu‘Zonal Buyer-Seller Forums’, lengo ni kukuza biashara na uwekezaji kuanzia kwenye ngazi za mikoa na wilaya.

“Lengo letu ni kuongeza mauzo baina ya biashara katika kanda zote nchini Tanzania. Kwa kushirikiana na kampuni ya kimataifa ya ushauri, Epvate & Fortune International Consulting (EFIC), TPSF pia itatoa tuzo na kutambua makampuni na mashirika binafsi (PSOs) ambayo yameonyesha utendaji wa kipekee ndani ya mwaka mzima,” anasema na kuongeza:

“Tutatoa zawadi kwenye vipengele vya vyama vya biashara vyenye michango maalum kwenye sekta, kampuni yenye shughuli bora zaidi za kusaidia jamii (CSR), kampuni inayochipukia (Startup) yenye ubunifu zaidi, kampuni bora katika utunzaji endelevu wa mazingira na taasisi za serikali zinazowezesha biashara,” anasema Ngalula.

WANAYOJIVUNIA

Tangu aingie madarakani, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa uwepo wa uhusiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi na kwamba ni muhimu kusherehekea mafanikio makubwa ambayo tasnia ya sekta binafsi imeyaona yakiwemo mambo kadhaa.

Limo, uchumi unavyokuwa kutoka kwenye kishindo cha maradhi Uviko-19,  ikimaanisha kwamba ukuaji uchumi nchini unakuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita licha ya kuwepo janga la uviko 19.

Jingine, ni kufufua sekta ya utalii nchini; Mwenyekiti akisema Filamu ya ‘The Royal Tour’ inatoa majibu kwa kuongeza watalii , kwani tangu Januari hadi Julai 2022, jumla ya watalii 742,133 walitembelea nchini ikiwa ni ongezeko la watalii 285,867, sawa na 62.7 kwa kulinganisha na mwaka uliopita.

MAPYA KILIMO, BIASHARA

Pia, inatajwa suala la kukuza sekta ya kilimo kupitia mikopo nafuu. Hapo Ngalula anasema, baada ya maelekezo ya Rais Samia ya kushusha riba kwenye sekta ya kilimo, kumetoa majibu kadhaa ya kiuchumi.  

“Tumeshuhudia benki zetu kushusha riba, kwa mfano CRDB ilishusha kutoka asilimia 20 hadi asilimia tisa, NMB asilimia 10 hadi tisa, TADB asilimia 11 hadi tisa, hali iliyowezesha wadau wa kilimo kupata mikopo kwa unafuu na kukuza sekta ya kilimo sambamba na ajenda 10/30,”anasema.

Jingine ni kuridhia Mkataba wa Kujiunga na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), akiufafanua kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa kati ya nchi nane kuanza kuuza bidhaa zake katika eneo hilo, huku wakinufaika na punguzo za kodi.

Kingine ni kufungua masoko ya kimataifa, Rais amefanya kazi kubwa sana kufungua masoko ya kimataifa.

“Wafanyabiashara wa Tanzania sasa wanasafirisha parachichi kwenda, Afrika Kusini, India na hivi karibuni China. Mpaka 2023 tutaweza kusafirisha tani 15,000 zenye thamani ya Sh.103.5, ukilinganisha na tani 8,000 mwaka 2018.

“Pia tumeona soko kubwa la mbuzi kwenda Oman, Kuwait, Falme za kiarabu ambapo wafanyabishara mwaka 2022, wameweza kuuza zaidi ya Sh.bilioni 8 sawa na ongezeko la asilimia 25,” anasema.

Jingine linalojumuishwa ni kudhiti bei za mafuta kupanda kwa kutoa ruzuku, hali iliyosaidia kupunguza makali ya maisha.

Mwisho

==

  • Kikao kujadili dira ya biashara kikiendelea.
  • Hatua ikipigwa kwenye uzalishaji shambani. PICHA ZOTE: MAKTABA.
Source : Nipashe

SHARE THIS POST