Tukutane palepale, nikuonyeshe kazi

3 miezi imepita 37

Jumamosi, Desemba 31, 2022

By  Mwandishi Wetu

Mwananchi Communications Limited

VINARA wa Ligi Kuu Yanga jioni ya leo Jumamosi watakuwa ugenini kuikabili Mtibwa Sugar katika mechi ya kufunga mwaka 2022 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, huku ikiwakosa baadhi ya nyota wake.

Pambano hilo ni la 26 kwa vigogo hao katika ligi tangu mwaka 2010, huku rekodi zikionyesha Yanga ndio wababe wa mechi zao kwani katika mechi 25 za awali imeshinda 13, huku wenyeji Mtibwa ikitakata katika mechi tano tu na saba zilizobaki ziliishia kwa sare za aina tofauti.

Yanga pia kwenye mechi hizo 25 imekusanya jumla ya pointi 46 dhidi ya 22 za Mtibwa, huku ikifunga mabao 27 na kuruhusu 14, kitu kinchofanya mechi ya leo kuwa na mvuto kwa mashabiki wakitaka kuona kama Vijana wa Jangwani wataendeleza ubabe ama watazimwa kwa mara ya kwanza tangu 2019 ilipochapwa bao 1-0 mjini Morogoro.

Timu hizo zinakutana huku Yanga ikiwa kileleni ikikusanya pointi 44 katika mechi 18, wakati Mtibwa ikishika nafasi ya nane ikiwa na pointi 24.

Katika mechi ya msimu uliopita iliyopigwa Manungu, Yanga iliibuka mshindi wa mabao 2-0 na kwa msimu huu mchezo wa kwanza huu uliopigwa jijini Dar es Salaam, Mtibwa ilicharazwa mabao 3-0, huku ikiwa ni timu ya pili iliyoruhusu mabao mengi zaidi (29) ikiifuata Polisi Tanzania iliyofungwa 31.

Hivyo katika mechi ya leo Mtibwa itakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha hawatobolewi tena na wageni wao wenye kinara wa mabao, Fiston Mayele aliyefunga mabao 14 hadi sasa. Yanga haitakuwa na Bernard Morrison, Feisal Salum, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Denis Nkane na Khalid Aucho.

Aucho anasumbuliwa na misuli ya nyama za paja, Lomalisa ana jeraha ya nyonga, wakati Djuma anaumwa na Nkane aliumia kwenye mechi ya Coastal Union, wakati Morrison akidaiwa kuwa na matatizo ya kifamilia, wakati Fei Toto ana sakata lake la kuvunja mkataba na Yanga na kutimikia Zenji.

Wenyeji Mtibwa Sugar wanaingia katika mchezo wa leo wakiwa hawana mwenendo mzuri kwenye ligi. Timu hiyo inayonolewa na Kocha Salum Mayanga, tangu ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Novemba 21, imecheza mechi tano mfululizo bila kupata ushindi ambapo imetoka sare mara tatu na kupoteza mechi mbili. ikifunga mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba.

Kocha Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Awadhi Juma, alisema kuwa wapo tayari kukabiliana na Yanga.

“Tunafahamu Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri na imekuwa inaongoza ligi. Kwetu sisi Mtibwa tumejiandaa vizuri kukabiliana nao ingawa tunafahamu mechi haitokuwa rahisi,” alisema Juma.

Makocha wa pande zote mbili wametambiana kila mmoja akiamini timu yake itaibuka na ushindi, licha ya kukiri mchezo utakuwa mgumu kwa sababu ya upinzani wa timu hizo.

“Hautakuwa mchezo mwepesi, ukizingatia tunacheza ugenini, lakini tunaamini tutapambana na kutafuta ushindi kabla ya kwenda Mapinduzi Cup,” alisema Nasreddine Nabi. wakati Salum Mayanga wa Mtibwa alisema wamejiandaa kwa mchezo huo na dakika 90 zitaamua.

Mbali na mechi hiyo leo kuna mchezo mwingine utakaopigwa Azam Complex kwa wenyeji Azam kuikaribisha Mbeya City.

Source : Mwanaspoti

SHARE THIS POST