Watoto wenye mahitaji maalum kupimwa magonjwa yasiyoambukiza

2 miezi imepita 34

Ombi hilo limetolewa na wadau wa huduma dhidi ya watoto wenye mahitaji maalum mkoani Mbeya wakidai kuwa hatua hiyo itasaidia kuokoa maisha ya hao ambao wako hatarini kuugua magonjwa hayo.

Wamesema utafiti walioufanya umebaini kuwa kundi hilo hajafikiwa wala kufikiriwa kupewa huduma ya kuwakinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kutokana na aina ya ulemavu walionao, sambamba na baadhi ya wazazi au walezi wao kutokuwa na moyo wa kuwahudumia.

Meneja miradi wa shirika la kuhudumia watoto wenye ulemavu nchini CST, Hildergade  Mehrab ametoa kauli hiyo alipozungumza na Nipashe Digital kuhusu madhira wanayokabiliana nayo watoto wenye mahitaji maalum kwenye sekta ya afya.

Amesema maeneo yanayopaswa kushughulikiwa na serikali kwa kushirikiana na wadau ni kuandaa utaratibu maalum wa kuwafikia na kuwahudumia watoto wote wenye mahitaji maalum nchini kuwapima magonjwa yasiyoambukizwa.

Amesema hatua hiyo itawasaidia kuwalinda dhidi ya magonjwa hayo sambamba na kuwapatia tiba ili kuokoa maisha yao.

“Nimewahi kupata kisa cha  mtoto mmoja mwenye ulemavu ambaye aliugua kwa muda mrefu saratani na baadae alipoteza maisha laity angepimwa na kupata matibabu mapema angepata nafuu au kupona kabisa, huyo ni miongoni mwa watoto ambao huenda katika maeneo wanayoishi wanazo dalili au wanaugua magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza kama vile saratani, moyo na kisukari,”amesema Hildergade.

Ameongeza kuwa watoto wenye mahitaji wapo katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na mazingira waliyonayo kutowasaidia kupata huduma kwa urahisi ikiwemo wazazi au walezi kutotoa kipaumbele kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma, serikali kutoweka utaratibu maalum kwa ajili ya kuwasaidia.

Ofisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Christopher Msaghaa amesema tayari jitihada za kuhakikisha kundi hilo linapata huduma sahihi za matibabu.

Amesema jitihada hizo ni pamoja na kupima hali za lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambapo kupitia afua mbalimbali za lishe wanawapatia wazazi elimu ya lishe bora ili kupambana  na tatizo la utapiamlo.

Jitihada nyingine ni wizara ya Afya katika maeneo mbalimbali ya kutoa huduma za afya kutoa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa watoto wenye umri kuanzia miaka tisa mpaka 14 hatua hiyo pia inawajumuisha watoto wenye mahitaji maalum.

“ Ni jukumu la serikali kupitia wizara ya afya kuwapatia huduma muhimu za afya kwa kundi hilo, jitahada mbalimbali zimefanyika ikiwemo utoaji wa chanjo wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano lakini bado kuna uhitaji mkubwa wa upimaji  ugonjwa wa kisukari amesema Msaghaa na kuongeza:

Bado tuna uhitaji mkubwa wa rasimali fedha ili kufanikisha zoezi la upimaji  wa kisukari wa watoto wetu wenye mahitaji maalum ni eneo ambalo linahitaji nguvu ya ziada kwa kundi hilo wadau  watusaidie amesema Msaghaa.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST