Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Wikicha Estate Development Agency inayosimamia na kumiliki shughuli zote zinazofanywa kwenye kiwanja namba 48766 kilichopo Ukonga Banana jijini Dar Es Salaam inatarajiwa kuburuzwa mahakamani kwa madai ya kufanya uharibifu wa na wizi wa mali za mamilioni ya fedha.
Akizungumza na mwandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali jijini Dar es Salaam Wakili Frenk Chundu amedai wanakusudia kuishitaki kampuni hiyo kwa kitendo ilichokifanya cha uharibufu wa mali za mteja wake.
Amedai kitendo kilichofanywa na kampuni hiyo dhidi ya mteja wake cha kuvunja baa iliyopo kwenye kiwanja hicho iliyokuwa inajulikana kwa jina la Big Mountain sio cha kiuungwana na nikinyume na sheria.
“Ni kweli tulikuwa na kesi kati ya mteja wangu Big Mountain na kampuni hiyo ya Wikicha namba 131 ya mwaka 2021 iliyoamuliwa Desemba 19, 2022 katika Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Ilala. uamuzi wa baraza hilo uliipa ushindi Wikicha kwa kumtaka mteja wangu kuondoka kwenye eneo hilo.
“Wakati tunajipanga kukata rufaa kampuni hiyo ilifanya uvamizi kwenye baa hiyo usiku wa kuamikia Desemba 29,2022 kinyume cha sheria kwa kuendesha uvunjaji wa baa hiyo.Uvaunjaji huo ulisimamiwa na mmoja wa mjukuu wa mmiliki wa eneo hilo Wilson Chacha”.
Wakili huyo amedai baada ya tukio hilo kufanyika alifika eneo la tukio na kumshauri mteja wake atoe taarifa polisi na alifanya hivyo na kupewa RB namba STK/RB/12887/2022 ambapo.Mjukuu aliyesimamia uvunjaji huo aliyetajwa kwa jina la Godfrey ametoweka kusikojulikana na anatafutwa na Jeshi la Polisi.
Kwa upande wa walinzi wa Big Mountein Benedcto Joseph na Mathayo Baruti wamedai wakati wapo kwenye majukumu yao ya ulinzi walimuona Godfrey Chacha (mjukuu) akiwa na watu 10 wakiwa na mapanga na marungu ambao waliwazingira na kuwaweka chini ya ulinzi na kuwafunga kamba kisha kuwalaza chini.
Wamedai baada ya hapo Godfrey alikwenda kuzima umeme ndipo lilipofika kundi kubwa la zaidi ya watu 40 wakiwa na mapanga na mashoka sambamba na katapila lenye kijiko zikiongozana na kenta mbili huku namba za usajili zikiwa zimezibwa.
“Walianza kutoa vitu kwenye kanunta ya baa na kupakia kwenye magari yale wakisimamiwa na Godfrey Chacha pamoja na Mtanzania mwenye asili ya Kiarabu aliyekuwa anaamrisha wafanye haraka wasije wakakutwa na polisi”. Walisema."
Wamedai walipomaliza kupakia katapila lilianza kuvunja baa yote pamoja na myamvuli, jokofu, viti na mabago ya matangazo ya kampuni mbalimbali za vinywaji.
Kwa mujibu wa walinzi hao wamedai walipomaliza kutekeleza uvunjaji huo waliokuwa wamewekwa chini ya ulinzi walimrishwa wapande kwenye gari na kisha wakaondoka haraka eneo la tukio.
“Baada ya wavunjaji kuondoka wakiongozwa na Godfrey tuliomba msaada kwa akinadada wanaofanya biashara katika maeneo hayo ili watufungue kamba wakafanya hivyo, tukatoa taarifa kwa meneja wetu ambapo naye alitoa taarifa polisi usiku huo.
“Polisi walifika kwa haraka eneo la tukio na kujionea uharibufu huo ndipo walipoamua kumfata nyumbani kwake ambapo hata hivyo hawakumkuta," wamedai walinzi wa baa hiyo.
Hata hivyo wamiliki wa eneo hilo wanaendelea kutafutwa ili kupata ukweli wa tukio hilo la kudaiwa kufanya uharibifu wa mali.