Yanga kufurahia Unbeaten 49 J'pili

2 miezi imepita 33

Hatua hiyo imekuja ikiwa na machungu ya kupoteza mechi yake dhidi ya Ihefu SC iliyochezwa Jumanne iliyopita kwenye Uwanja wa Highland Estates ulioko Mbarali, Mbeya na kushindwa kufikisha 'Unbeaten' ya 50.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema kulikuwa na vitu viwili au vitatu ambavyo vilisababisha wakapoteza mechi hiyo huku akifunguka kabla ya mchezo huo, dalili za kufungwa zilianza kuonekana mapema.

Kamwe alisema licha ya Ihefu kutokuwa na msimu nzuri, lakini 'Walima Mpunga' hao wana kikosi imara kinachopambana lakini hakina bahati ya kupata ushindi.

"Kwanza ni uchovu, pili ni hali ya majeruhi, wachezaji wetu wengi wana fatiki, ulikuwa ukiwaona tu hata wanavyokimbia unaona hawaendi inavyotakiwa. Watu wengi hawajui idadi kubwa ya wachezaji wa Yanga ni majeruhi ambao wako nje na wengine wanacheza, unawaona tu uwanjani lakini hawako fiti kwa asilimia zote," alisema Kamwe

Alimtaka mshambuliaji, Fiston Mayele ni mmoja wa wachezaji ambao hawako fiti lakini analazimika kupambana ili kuisaidia timu kufikia malengo.

"Hata Salum Aboubakar 'Sure Boy' hivyo hivyo, Khalid Aucho naye pia ni majeruhi, walijituma kwa sababu tu wanaipenda Yanga na wanapenda mashabiki wapate burudani, walipambana ili timu ipate matokeo, lakini hawakuwa fiti," alisema Kamwe.

Aliitaja sababu nyingine ambayo iliwakosesha ushindi ni namna Ihefu ilivyodhamiria kupata ushindi katika mechi hiyo kutokana na mikakati waliyokuwa nayo kuelekea mchezo huo.

"Unajua hizi timu ndogo zikiwa zinataka kucheza na timu kubwa, lengo lao la kwanza huwa ni mapato ya mlangoni, ndiyo maana unaona timu inaweza kuwa na makazi Dar es Salaam, lakini ikapeleka mechi yake Kigoma, inachotaka ni kupata mashabiki wengi kwa sababu mikoani watu wengi wanajazana viwanjani kuziona timu kubwa, pointi tatu huwa ni lengo lao la pili," alisema kiongozi huyo.

Aliwataja wachezaji walikosekana katika mechi hiyo ambao ni Bernard Morrison na Feisal Salum 'Fei Toto' tayari wameshapona na wanachofanya sasa ni kufanya mazoezi ya utimamu wa mwili, ili warejee kwenye majukumu yao baada ya ripoti ya madaktari kuwaruhusu.

"Wale waliodhania baada ya kufungwa tutachanganyikiwa au wamepata pa kusemea wanajidanganya, tunakwenda kufanya sherehe kwa ajili ya kucheza mechi 49 bila kupoteza. Tuna sababu ya kujivunia, tuna sababu ya kusherehekea. Kutakuwa na keki siku ya Jumapili kwenye mechi dhidi ya Prisons, kutakuwa na wasanii watakaotumbuiza," Kamwe aliongeza.

Mara ya mwisho Yanga kupoteza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ilikuwa Aprili 25, mwaka jana na ilichapwa bao 1-0 na Azam FC.

Viungo Never Tegere na Lenny Kissu wa Ihefu ndiyo waliohitimisha 'unbeaten' hiyo.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST