YANUIA ‘KUTEKA’ 44%  INAYOAGIZWA …

2 miezi imepita 58

Changamoto hiyo ya uhaba wa mafuta ya kula ilitokana na upungufu wa uzalishaji na kutegemea uagizaji mafuta ya kula nje ya nchi. Bei ya mafuta ya kula hutegemea soko la bidhaa hiyo kulingana na msimu na mabadiliko ya bei katika soko la dunia.

Serikali ilichukua hatua kukabiliana na tatizo, kwa kuzipatia leseni kampuni mbili za uagizaji wa mafuta ya kula kwa mwaka.

Mahitaji ya mafuta ya kupikia nchini kwa mwaka ni wastani wa tani 600,000 hadi 700,000 wakati kiasi kinachozalishwa nchini kinatajwa kuwa tani 205,000 kwa mwaka.

Singida ni kati ya wazalishaji wakubwa wa mafuta ya kula, katika orodha ya mikoa 11 nchini inayozaliosha bidhaa hiyo, mafuta ya alizeti yaliyo juu zaidi kisoko. Sasa nao umeamua kushiriki kuziba pengo hilo la mafuta ya kula nchini, kwa kuongeza uzalishaji wake.

Mikoa mingine inayolima alizeti kwa wingi ni: Shinyanga, Dodoma, Iringa, Tabora, Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Arusha, Manyara, na Rukwa inakolimwa kwa ajili ya chakula na biashara.

Miongoni mwa mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula ya alizeti iliyowekwa na mkoa wa Singida, ni kuhakikisha uzalishaji wa mafuta hayo unafikia tani 159,110.5 sawa na asilimia 44.2 ya mafuta yanayoingizwa nchini.

Mkakati huo unalenga kuisaidia nchi kuondokana na tatizo la upungufu wa mafuta ya kula ambao utaanza kutekelezwa katika msimu uliopo sasa na mavuno yake kushuhudiwa mwakani.

MKAKATI MKOA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mkakati ya Kuongeza Uzalishaji wa Alizeti Mkoa wa Singida, Justice Kijazi, anakieleza kikao chini ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alipokuwa ziara mkoani hapa.

Kijazi anasema, ili kufikia uzalishaji huo wa mafuta mkoa umepanga kuongeza eneo la kulima alizeti ambazo zitalimwa ekari 631,391 kwa matarajio ekari hizo zitazalisha tani 492,485 za alizeti.

Anafafanua kuwa, ili kufikia uzalishaji huo, mkoa utahitaji tani 1,262.5 za mbegu bora za alizeti aina ya Certified 1.

Hadi sasa anasema, mkoa Singida una jumla ya viwanda 221 vya kusindika alizeti, vinavyohitaji tani 635,465 kwa mwaka. Lakini, kwa kipindi cha miaka mitano sasa, kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi msimu uliopita, uzalishaji wa alizeti haujawahi kuvitosheleza viwanda hivyo.

Katika kipindi chote hicho uzalishaji wa juu ulikuwa ni tani 260,064 na msimu uliopita (2021/2022) hali haikuwa nzuri.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, anasema mkoa sasa umetengewa kilo 500,000 za mbegu bora za alizeti ya ruzuku zenye thamani ya Sh. bilioni mbili katika msimu uliopo wa kilimo, ambao sasa wakulima wanaandaa mashamba.

Anasema mbegu hizo aina ya Certified 1 zitauzwa kwa wakulima kwa bei ya Sh.5,000 kwa kilo, badala ya Sh.8,000 kwa kuwa zina ruzuku ya serikali.

Serukamba anasema serikali pia imetoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wote watakaojiandikisha kwenye mfumo maalum wa kupata ruzuku, ambao kwa sasa usajili unaendelea katika halmashauri zote saba za mkoa wa Singida.

WAZIRI BASHE

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, anasema katika kuunga mkono kilimo hicho cha alizeti, serikali katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao inatarajia kutenga Sh.bilioni 4.6 kwa ajili ya kununua zana za kilimo za kuunga mkono mkoa Singida, lengo ni kuinua kilimo mkoani hapo.

Anasema, baada ya kununuliwa zana hizo, halmashauri husika zitatakiwa zitenge maeneo maalumu ambako zana itawekwa na kutakuwepo mtu maalum wa kuzisimamia, ambako wakulima watakuwa wakienda kuzikodisha.

Kwa mujibu wa Waziri Bashe, fedha zitakazopatikana baada ya wakulima kukodi zana hizo, zitarudishwa serikalini na kwenda kununua zana kwa ajili ya mikoa mingine.

Kuhusu upatikanaji mbegu za alizeti, Bashe anasema mwelekeo wa serikali sasa ni kuweka nguvu kwenye utafiti na uzalishaji wa mbegu, upatikanaji pembejeo na huduma za ugani.

Anasema, ili kuondoa tatizo la mafuta nchini tunahitaji tuwe na tani 15,000 za mbegu bora ya alizeti, mwaka jana zilizalishwa tani 223 tu na msimu uliopo uzalishaji mbegu zaidi utafanyika kuchochea uzalishaji alizeti shambani.

KUTOKA TARI

Kwa mujibu wa Bashe, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imepanga kuanzisha shamba darasa la zao alizeti katika mkoa wa Singida, ambako mbolea za aina zote zitatumika kuleta ufanisi kwenye zao hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Geofrey Mkamilo, ametangaza mpango huo wakati wa uzinduzi wa msimu wa kilimo mwaka 2022/2023 na ugawaji wa mbegu za alizeti zenye ruzuku zilizotolewa na serikali.

Anasema TARI itaanzisha shamba darasa hilo ili kupima afya ya udongo kwani zipo mbolea za aina mbalimbali ambazo zitatumika katika zao la kimkakati kama alizeti ili kuona zinaleta ufanisi gani kwenye zao hilo.

Dk. Mkamilo anasema TARI kwa kushirikiana na sekretarieti ya mkoa wa Singida na Wizara ya Kilimo, kutoa mafunzo kwa maofisa ugani na wakulima ili kuongeza tija na uzalishaji wa zao la alizeti.

Kuhusu upatikanaji mbegu, anasema TARI itaendelea kushirikiana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuzalisha mbegu za kutosha hususani za zao la kimkakati la alizeti.

"Tayari tumeshakubaliana kiasi cha mbegu ya alizeti kinachohitajika ambacho TARI itazalisha kwa ajili ya kumpa ASA, ili waweze kuzalisha madaraja bora ambayo yatawafikia wakulima ili wakulima waweze kuongeza tija na uzalishaji wa alizeti," anafafanua.

Dk.Mkamilo anasema suala la viuatilifu, TARI itahakikisha vinaangaliwa kisayansi namna gani vitaondoa wadudu.

Source : Nipashe

SHARE THIS POST